Viongozi wa kisiasa walioasi muungano wa Cord wamepewa nafasi ya kuandika barua za kujiuzulu rasmi kutoka katika chama hicho cha upinzani.
Akiongea kwenye kituo kimoja cha redio nchini siku ya Jumatano, katibu mkuu wa muungano wa Cord Ababu Namwamba, alisema kuwa ni kinyume cha sheria kwa baadhi ya viongozi waliochaguliwa na rai kwenye mrengo fulani wa chama, kumfanyia kampeni mgombeaji kiti wa chama pinzani.
Aliwataka wahusika kubeba mzigo huo na kuwajibikia wapiga kura waliowachagua kwa kujiondoa na kusimama upya kutumia chama cha JAP ambacho alisema walikuwa wakipigia debe huko Malindi.
Ababu aliwataka viongozi hao kuiga mfano wa kiongozi wa muungano huo Raila Odinga, ambaye amewahi kujiuzulu rasmi baada ya kugura kutoka chama cha Ford Kenya, na kusimama upya kwenye kiti cha ubunge cha Lang’ata na kuchaguliwa upya.
Aidha, mbunge huyo wa Bundalangi aliipa changamoto Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC, kufanya uchunguzi kuhusiana na visa vya maafisa wa serikali kutumia rasilimali za umma kufanyia kampeni, hatua aliyosema kuwa ni kinyume cha sheria.
Baadhi ya viongozi kutoka mrengo wa upinzani ambao wameonekana wazi wazi wakifanya kampeni kwenye upande wa serikali ni pamoja na mwakilishi wa wanawake wa Kaunti ya Kwale Zeinab Chidzuga, Mbunge wa Kilifi Kaskazini Gideon Mung’aro, na mwenzake wa Kilifi Kusini Mustafa Iddi miongoni mwa wengine.