Share news tips with us here at Hivisasa

Viongozi wa mitaa na jamii kwa jumla wamehimizwa kusaiadia katika vita dhidi ya ubakaji na kutoa habari kuhusiana na wabakaji katika mitaa wanamoishi ili kuhakikisha kuwa visa kama hivyo vya ubakaji vinatokomezwa.

Akiongea na waandishi wa habari siku ya Alhamisi kwenye maandamano eneo la Kisauni jijini Mombasa, afisaa wa kushughulikia masuala ya jinsia katika shirika la kutetea haki za binadamu la Muhuri, Topster Juma alisema kuwa viongozi sharti wawe na mtazamo komavu kuhusiana na masuala ya unajisi wa  watoto kwenye maeneo wanayosimamia.

Alisema kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakitetea wahalifu pamoja na wahusika katika visa vya ubakaji hali ambayo inafanya mchakato mzima wa kupiga vita jinamizi hilo kuwa vigumu ambapo aliwataka viongozi kuja pamoja kuendeleza juhudi za pamoja kuzika zimwi hilo.

Amesema haya baada ya mtoto mmoja wa miaka 12 kunajisiwa na mwanamme ambaye anajulikana katika eneo la Kisauni ambapo inadaiwa kuwa juhudi za kupata haki ya mtoto huyo msichana imekuwa vigumu kwa sababu ya wanaohusika kwenye kutekeleza sheria kudinda kumchukulia hatua za kisheria mhusika.

Baadhi ya wakazi ambao walishiriki kwenye maandamano siku ya Alhamisi wametaja idara ya polisi kuwa ya kujikokota kushughulikia visa hivyo vinavyoripotiwa kituoni na pia kudai kuwa baadhi ya viongozi wa mitaa nao wamekuwa vikwazo kwenye harakati hizo za kutafuta haki za waathiriwa.