Viongozi wa kisiasa wanawake mjini Mombasa wamehimizwa kuitekeleza miradi ya maendeleo kwa wakazi baada ya kuchaguliwa, badala ya kuhusika katika siasa za malumbano ya mara kwa mara.
Akizungumza afisini mwake mjini Mombasa siku ya Alhamisi, mwenyekiti wa chama cha Maendeleo ya Wanawake, Bi Afiya Rama, alisema ni jambo la kushangaza kuwaona wanawake pamoja na vijana wakihangaika wakati viongozi waliowachagua kuwatetea wakizifumbia macho shida zinazowakumba.
Alisema kuwa viongozi hao badala yake wanashinda wakivihama vyama moja hadi nyingine kujinufaisha.
“Viongozi wanawake siku hizi wamekua tu kama wanaume. Hawajali changamoto zinazo wakabili wanawake wenzao, imekua tu ni siasa kila mahali,” alisema Rama.
Aidha, Rama amewahimiza wanawake na vijana kujiunga katika makundi ili waweze kuchukua mkopo kwa serikali, hatua anayosema itawapa uwezo wa kufungua biashara zao na kujiendeleza kimaisha bila kuutegemea usaidizi wa mtu mwingine.