Mamlaka ya kitaifa ya usafiri na usalama barabarani, NTSA imehimiza viongozi kuwacha kuingiza siasa katika swala la ujenzi wa eneo la kuegesha magari kwenye barabara ya Salgaa.
Kupitia kwa taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Jumatano, mwenyekiti wa NTSA Lee Kinyanjui alisema eneo la kuegesha magari lililostahili kujengwa mwaka jana halikujengwa kutokana na tofauti baina ya viongozi na wakaazi wa eneo hilo.
Kinyanjui alisema kuwa ujenzi huo uliostahili kufanywa kwa ushirikiano na mamlaka ya Kenya National Highways Authority (KENHA), serikali ya Kaunti ya Nakuru pamoja na wafadhili wengine haukuanza kutokana na ukosefu wa makubaliano kuhusiana na mahala ambapo eneo hilo lingejengwa.
“Eneo hilo la uegeshaji magari lilikuwa lina lengo la kuegesha malori ya kubeba mafuta ili kuzuia msongamano unaoshuhudiwa kwa sasa katika kituo cha kibiashara cha Salgaa. Hatua hiyo pia ingezuia matukio ya kuzuka kwa moto,” alisema Kinyanjui.
Akiangazia baadhi ya hisisa zilizoibuka kutokana na ajali ya mkesha wa kuamia mwaka mpya katika eneo la Salgaa pamoja na ajali iliyotokea tarehe moja Januari, mwenyekiti huyo wa NTSA alidokeza kwamba eneo hilo la uegeshaji wa magari lina lengo la kupunguza msongamano na ajali ambazo huzuka mara kwa mara katika eneo hilo la Salgaa.
Hata hivyo, alidhibitisha kwamba mamlaka husika ziko katika harakati za kukagua eneo ambalo litatumika katika ujenzi wa eneo hilo la kuegesha magari.
Wakati huo huo, amehimiza mamalaka husika kudhibiti vilabu na maeneo ya kujivinjari yanayoanzishwa kwenye kituo cha kibiashara cha Salgaa kilicho kandokando mwa barabara kuu ya Nakuru-Eldoret.
Kinyanjui aidha alishtumu madereva wanaotumia barabara hiyo ya Salgaa yenye umbali wa kilomita 12 kwa kuendesha magari yao kwa kasi bila kujali wanaotumia barabara hiyo, pamoja na kuendesha magari hayo wakiwa walevi.