Maafisa wa usalama mjini Mombasa wamesema kwamba watazidisha vita dhidi ya walanguzi na watumizi wa mihadarati hadi pale watakapojisalimisha.
Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Nelson Marwa amesema kwamba kupitia juhudi hizo, tayari walanguzi wakuu wa mihadarati wameanza kujisalimisha kwa maafisa wa usalama na kukiri kusitisha kuendeleza biashara hiyo haramu.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Marwa alisema kwamba mlanguzi mkuu wa dawa za kulevya katika eneo la Pwani Said Mohammed Swaz, alijisalimisha kwa maafisa wa polisi na atasaidiana na maafisa hao kuwakabili walanguzi wengine wakuu.
Wakati huo huo, amewataka wazazi wa vijana waliojiunga na makundi ya kihalifu ya 'Wakali Kwanza' na 'Wakali Wao' kuwashauri kujisalimisha kwa maafisa wa polisi ili kujumuishwa katika shirika la huduma kwa vijana NYS, la sivyo maafisa wa polisi watawakabili.
"Tunawaomba wazazi wa vijana walijiunga na makundi ya kihalifu kuwashauri watoto wao kujisalimisha mara moja kwa maafisa wa polisi, kabla ya vijana hao kukabiliwa kikamilifu. Vijana hao wamechangia kukithiri kwa ukosefu wa usalama,” alisema Marwa.
Idara ya usalama katika Kaunti ya Mombasa imeahidi kuzuru hadi mashinani na kuwakabili walanguzi wa mihadarati pamoja na wahalifu wanaochangia kuvuruga usalama wa Kaunti.