Wahudumu wa matatu katika kaunti ya Nakuru wana kila sababu ya kutabasamu baada ya serikali ya kaunti kuanzisha mpango wa kukarabati na kupanua kituo cha uchukuzi cha Mashambani.
Gavana wa Nakuru Bw Kinuthia Mbugua alisema kuwa upanuzi huo utagharimu milioni 13.
Alisema kuwa ujenzi huo utafanywa kwa ushirikiano na shirika la Kenya Roads Board (KRB) ambao utafanyika kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Gavana Mbugua alitaja mashimo barabarani kama changamoto kuu ambayo imesababisha uharibifu mkubwa wa baadhi ya barabara za kaunti.
“Mashimo madogo madogo barabarani yasiposhughulikiwa yakiwa katika hali hii, hatimaye hupanuka na kusababisha uharibifu mkubwa haswa kwa magari ya uchukuzi,” alisema Bw Mbugua.
Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Avery East Africa Ltd Nicholas Kithinji alisema kuwa Nakuru itakuwa kaunti ya kwanza kufanyiwa jaribio la teknolojia hiyo mpya.