Vuguvugu la 'Pwani ni Kenya' sasa linamtaka Rais Uhuru Kenyatta amfute kazi mkurugenzi wa huduma za Feri Musa Hassan kwa kile walikitaja kama hatua ya kipekee itakayosaidia kuimarisha huduma za Feri ya Likoni.
Wakiongozwa na mwenyekiti wao Alex Kasuku, wanachama wa vuguvugu hilo walidai kuwa mkurugenzi huyo ameshindwa na kazi huku wakitaja msongamano wa mara kwa mara unaoshuhudiwa katika kivukio cha Feri cha Likono kama dhihirisho tosha kuwa Hassan ameshindwa kuwajibika.
''Tunamshukuru Rais kwa kuzuru eneo la Feri, tunatumai alijionea hivyo tunamwomba afanye mabadiliko kabla hajarudi Nairobi. Amtimue huyo mkurugenzi na kikosi chake'' Kasuku alisema.
Siku ya Jumatatu Rasi Kenyatta alizuru eneo la Feri ya Likoni na kuonyesha kughadhabishwa kwake na huduma mbovu zinazotolewa na wasimamizi japo alisema huenda kuzeeka kwa baadhi ya mashua kunachangia hali hiyo.
Hata hivyo, Kasuku, amenukuliwa katika jarida moja la humu nchini akisisitiza kuwa lazima mkurugenzi huyo afutwe kazi akidai hawezi kuimarisha hali katika kivukio hicho.
Msongamano wa mara kwa mara unaokumba wasafiri wanaotegea huduma za Feri ya Likoni umemtia lawamani mkurugenzi wake Musa Hassan huku baadhi ya viongozi mkoani Pwani akiwemo kamishna wa kaumti ya Mombasa Nelson Marwa wakipendekeza atimuliwe.
Hata hivyo huenda hali hiyo ikapata suluhu ya kudumu baada ya waziri wa utalii Najib Balala wiki iliyopita kusema kuwa serikali itafadhili ujenzi wa kivukio cha kisasa ili kurahisisha shughuli za usafiri.