Miungano ya vyama vya kutetea maslahi ya wafanyikazi katika kaunti ya Uasin-Gishu chini ya mwavuli wa shirikisho la wafanyikazi nchini COTU inalaumu maafisa wa serikali wa leba katika kaunti ya Uasin-Gishu kwa kula njama na waajiri ili kunyanyasa wafanyikazi.
Miungano hiyo inadai kuwa maafisa hao wamezembea katika utendajikazi wao wa kutetea maslahi ya wafanyikazi.
Wakiongozwa na mwakilishi wa COTU katika kaunti hiyo Peter Odima walidai kuwa maafisa hao hupokea hongo kutoka kwa waajiri ambapo huwa vigumu kwao kushughulikia maslahi ya wafanyikazi kisheria.
“Ni aibu kuona kwamba wale watu ambao wanapaswa kutetea maslahi ya wafanyikazi ndio wanatumiwa na waajiri kuendeleza dhuluma dhidi ya wafanyikazi katika kaunti hii, hatutavumilia tabia kama hiyo,” alisema Odima.
Akihutubia wana habari mjini Eldoret Odima alionya kwamba huenda wafanyikazi wakatumia mbinu mbadala kulazimisha maafisa husika kuhama au kujiuzulu kutoka katika kaunti hiyo.
Odima alisema chama chake kitashinikiza maafisa husika kurekebisha tabia la sivyo wahamishwe kutoka katika kaunti hiyo.