Share news tips with us here at Hivisasa

Walimu katika kaunti ya Kisumu wametakiwa kufanya kazi kwa pamoja na viongozi wa miungano ya kutetea haki zao kama njia moja ya kuafikia matakwa yao kitaifa.

Katibu mkuu wa muungano wa waalimu katika kaunti ya Kisumu Joshua Ogalo alisema ni sharti viongozi wapya waliochaguliwa wafanye kazi kwa pamoja ili kuupa nguvu muungano huo.

Ogalo aliwataka wale walioshindwa kwenye uchaguzi wa kuwachagua viongozi wa KNUT siku chache zilizopita kukubali matokeo na kufanya kazi kwa pamoja na wale waliochaguliwa kuwa viongozi.

Alitoa wito kwa wote waliogombea nafasi za uongozi kwenye muungano wa KNUT Kisumu kushirikiana na kwa pamoja bila kujali aliyeshinda na aliyeshindwa.

Ogalo alisema: ''Kutoshinda katika kinyanganyiro chochote cha uchaguzi ni sawa na kushinda uchaguzi maana hali kama hii hutoa fursa ya mhusika aliye na azma ya kushiriki uchaguzi ujao kuwa tayari na kujipanga vyema hata zaidi.''