Waathiriwa wa ugonjwa wa kifua kikuu kwenye kaunti ya Nakuru na katika taifa nzima kwa ujumla wamehimizwa kujiunga na ukurusa wa Facebook uliaonzishwa kuwezesha kutoa maelezo kuhusiana na safari yao ya kupambana na ugonjwa huo.
Ukurasa huo unaofahamika kama Tb Photovoice kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook kwa muujibu wa Alice Opiyo, mmoja wa wanaofanya kazi katika shirika la KANCO (Kenya Aids NGOs Consortium), linaloangazia magonjwa kama vile maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Alisema kuwa ukurasa huu ulibuniwa baada ya kubainika kuwa kando na hitaji la dawa, waathiriwa hao pia wanahitaji nafasi ya kuelezea maswala mbalimbali yanayowakumba ambayo hawawezi kuyazungumzia kwa urahisi.
Opiyo, anayeshughulikia pakubwa maswala ya ugonjwa wa kifua kikuu anasema kwamba waliona umuhimu wa kubuni ukurasa huo wa Facebook kwa waathiriwa hao wa ugonjwa wa kifua kikuu ili wauguzi wanaowahudumia waweze kubaini njia mwafaka za kuweza kuwapa huduma kwa njia bora zaidi.
Kupitia kwa mahojiano na mwandishi huyu Jumatatu hii mjini Nakuru, waathiriwa hao wa ugonjwa wa kifua kikuu hutumia picha wanazozipiga wenyewe kuelezea safari yao ya kukabiliana na ugonjwa huo pamoja na maelezo kuhusiana na picha hizo wanazozipiga.
Izingatiwe kuwa shirika la TbPhotovoice lilianzishwa na Jamaa kwa jina la Romel Lacson mwaka wa 2004 baada yake kumpoteza mke wake na mtoto wake kutokana na matatizo yaliyotokana na ugonjwa wa kifua kikuu.