Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Hatua ya Kufungwa kwa kampuni mbili zinazomilikiwa na familia ya Gavana wa Mombasa Hassan Joho imetajwa kuwa za kiimla na baadhi ya wabunge wa eneo la Pwani ambao wanaegemea upande wa upinzani.

Wakizungumza wikendi na waandishi wa habari katika jiji la Mombasa, wabunge hao waliitaja hatua hiyo kuwa yenye nia mbaya na yenye malengo fiche.

Wakiongozwa na mbunge wa Kisauni Rashid Bedzimba na mwenzake wa Mvita Abdulswamad Nassir, wabunge hao waliitaja serikali ya Jubilee kama yenye mbinu za miaka ya zamani ambazo zilitumiwa na viongozi kuwanyamazisha wapinzani wao.

Bedzimba kwa upande wake alilitaka Shirika la Bandari nchini KPA, kukoma kutumiwa vibaya na serikali kwa maslahi ya kibinafsi, na kuwataka wahusika kuhakikisha kuwa mashirika hayo mawili ya Portside na Autoport Container Freight yanafunguliwa haraka iwezekanavyo.

‘Tunalitaka shirika la Bandari kufanya hima na kufungua mashirika hayo mawili badala ya kuwanyima haki Wakenya wengine kazi ambayo wanategemea kuwapa riziki yao ya kila siku,” walisema viongozi hao.

Walishangaa ni vipi shirika la Bandari lingeweza kufunga mashirika hayo bila fahamu yoyote ya wamiliki wa mashirika hayo.

Waliisuta serikali kwa kufunga mashirika hayo na kuwanyima zaidi ya watu 1000 ambao wamekuwa wakihudumu kwenye mashirika hayo ajira.