Share news tips with us here at Hivisasa

Kufuatia ongezeko la waathiriwa wa dawa za kulevya katika Kaunti ya Mombasa, sasa viongozi mbalimbali wanashinikiza wabunge kujenga vituo vya kurekebisha tabia.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumapili, mmoja wa wakurugenzi wa shirika la kupambana na mihadarati na vileo nchini Nacada Sheikh Juma Ngao amesema kwamba zaidi ya vijana elfu 25 Kaunti ya Mombasa wameathirika na utumizi wa mihadarati.

Ngao amependekeza wabunge wa eneo la Pwani kutumia fedha za hazina ya ustawishaji wa maeneo bunge CDF, na kutenga shilingi milioni 20 kila eneo bunge ili kujenga vituo hivyo na kuwanasua vijana.

“Tunawahimiza wabunge wa bunge kutenga fedha za CDF kujenga vituo vya kurekebisha tabia watumizi wa mihadarati kwani asilimia kubwa ya vijana mjini Mombasa wamejitosa na utumizi wa dawa za kulevya,” alisema Ngao.

Kaunti ya Mombasa imekuwa ikiangaziwa pakubwa kutokana na janga la mihadarati ambalo kwa miaka mingi limekuwa donda sugu.