Wachuuzi mjini Nyamira wameomba serikali ya kaunti kuwajengea soko la kisasa mjini humo.
Wachuuzi hao walisema kuwa hatua hiyo itaimarisha biashara miongoni mwao na kupunguza visa vya ajali barabarani wanapofanya biashara zao.
Wallisema kuwa ikiwa watajengewa soko hilo, biashara zao zitaimarika ipasavyo, na kuinua uchumi wa kaunti.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Nyamira siku ya Jumatano, wachuuzi hao wakiongozwa na Gladys Osinyo, walisema kuwa ujenzi wa soko hilo utawahakikishia usalama wanapofanya biashara zao.
“Tumekuwa tukilipa ushuru lakini kwa upande wetu hatuoni manufaa ya kulipa pesa hizo,” alisema Osinyo.
Aliongeza, “Tunaomba serikali itujengee soko hapa Nyamira ili tuweze kuimarisha biashara zetu. Soko hilo linaweza kupewa jina la ‘Soko la wachuuzi mjini Nyamira.”
Wachuuzi hao aidha walitaka serikali ya Kaunti ya Nyamira kuimarisha mazingira mjini Nyamira na kutowafukuza mjini humo kabla ya kuwajengea soko.