Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Naibu mwenyekiti wa chama cha Maendeleo ya Wanawake katika Kaunti ya Nyamira amewaomba washikadau mbalimbali na viongozi katika eneo la Kisii kujitokeza kusaidia akina mama kujiendeleza kimaendeleo.

Akizungumza siku ya Jumatano mjini Nyamira, Jerusha Momanyi alisema siku ya Ijumaa kutakuwa na sherehe ya kuwachangia akina mama hao pesa katika shule ya msingi ya Nyamira, huku akiomba wengi kujitokeza ili kuwafadhili akina mama kifedha.

Momanyi alisema chama cha maendeleo ya wanawake katika kaunti hiyo kimekuwa na ukosefu wa pesa na kuomba msaada.

“Siku ya Ijumaa tutakuwa na mkutano wa kuchangisha fedha ambazo zitasaidia chama chetu kuendelea. Naomba washikadau na viongozi wahudhurie sherehe hiyo ili watusaidie,” alisema Momanyi.

Aidha, aliwashauri wanawake katika kaunti hiyo kujiandikisha kwa chama hicho ili kutafuta njia ya kujiendeleza na kupunguza hali ya umaskini katika kaunti hiyo.

Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa wanawake wengi katika kaunti ya Nyamira bado hawajajiandikisha kwa chama hicho, jambo ambalo linadaiwa kurudisha maendeleo nyuma na kuleta umaskini.

Kulingana na mwenyekiti wa chama hicho katika Kaunti ya Nyamira Mary Orwenyo, wanawake 200 pekee ndio wamejiandikisha kwa chama hicho.