Share news tips with us here at Hivisasa

Wadau wa sekta ya utalii nchini wamehimiza ushirikiano na kuweka juhudi za kuboresha sekta hiyo kimataifa licha ya kukumbwa na changamoto na kusambaratika hapo awali.

Waziri wa Utalii katika kaunti ya Kwale Adam sheikh, alisema kuwa juhudi hizo zinafaa kuungwa mkono kikamilifu kwani zinahitaji muda wa kutosha kwani sekta hiyo ndio kitovu kikuu cha biashara nchini sambamba na kuwa kiegezo muhimu cha uchumi.

Akiongea na wanahabari siku ya Ijumma baada ya kukutana na wadau wa sekta hiyo mjini Mombasa, Bw Adam alisema kuwa matumaini ya kuimarika kwa sekta ya utalii yapo kwa kiwango kikubwa kwani idadi ya wageni wanaozuru ukanda wa Pwani imeongezeka.

“Kuna haja ya kuungana na wadau wote wa sekta ya utalii nchini kuhakikisha kuwa sekta ya utalii inaboreshwa zaidi ili kurejea katika hali yake ya hapo awali kwani sekta hii ndio tegemeo kubwa nchini kiuchumi," alisema Adam.

Kando na hayo, Adam aliitaka serikali kuu kuharakisha ujenzi wa barabara ya Samburu-Kwale itakayowawezesha wageni kufika eneo la Kusini mwa Pwani kwa haraka bila ya kukumbana na changamoto za kivuko cha feri.