Waziri wa Utalii nchini Najib Balala amewahimiza wadau wa sekta ya utalii nchini kushirikiana kwa karibu mno na serikali katika kuimarisha sekta hiyo.
Kulingana na Balala, iwapo wadau hao watajitolea kikamilifu na kuisaidia serikali kuliuza taifa hili katika nchi za magharibi basi kwa kiasi kikubwa sekta hiyo itaimarika na kurejea kama ilivyokuwa hapo awali.
Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumapili baada ya kuzuru katika maeneo ya kitalii mjini Watamu, Balala alisema kuwa uimarishaji wa sekta ya utalii kutawavutia wawekezaji wengi pamoja na wageni kutoka nchi tofauti na kukuza uchumi wa nchi.
"Tunawaomba wadau wa sekta ya utalii nchini kujitokeza waziwazi na kushirikiana na serikali katika kuimarisha sekta ya utalii ili kuona kwamba juhudi za kuboresha sekta hiyo na kuwavutia wageni wengi nchi zinafaulu," alisema Balala.
Amesema kuwa shilingi bilioni 5.2 zilitengewa wizara hiyo kwa kiwango kikubwa kusaidia kuboresha tamaduni za Wapwani na maeneo mengine ya kitalii nchini kama njia moja wapo ya kuekeza uchumi wa nchi.
Hata hivyo ameihimiza wizara ya uchukuzi na miundo msingi nchini kuhakikisha kuwa inakamilisha ukarabati wa barabara ili kuwawezesha watalii wanaozuru nchini kutokumbwa na changamoto.