Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wadau mbalimbali katika sekta ya afya Mombasa wanaitaka serikali ya kaunti kuharakisha mpango wa kujenga kituo cha kurekebisha tabia kwa watumizi wa mihadarati eneo hilo.

Wadau hao kutoka mashirika mbalimbali ya kijamii wanashangazwa na jinsi ambavyo kaunti ya Mombasa inakosa kituo kama hicho ikizingatiwa kwamba ni moja kati ya maeneo ambayo yameathirika zaidi na janga hilo humu nchini.

Akiongea mjini humo siku ya Ijumaa katika semina maalum, mshirikishi wa Teens Watch Cosmas Maina aliitaka serikali ya kaunti kuhakikisha mpango huo unakamilika mwaka huu.

“Ni jambo la kushangaza kwamba eneo letu halina kituo hiki muhimu, ni jukumu la kaunti kuharakisha zoezi la kujenga sehemu hii angalau tufanikishe hivi vita vya madawa ya kulevya,” alisema Maina.

Kwa upande wake mwakilishi mteule katika bunge la Mombasa Bi Mary Akinyi alitoa ahadi kwamba hoja ya kufanikisha mpango huo ni moja kati ya hoja zinazotarajiwa kujadiliwa bungeni mwaka huu.

“Tuko na mswada wa afya ambao hivi karibuni utajadiliwa bungeni na moja kati ya mambo muhimu ni kuanzisha kituo hicho,” alisema Bi Akinyi.

Aidha mwakilishi huyo ambaye pia ni mshirikishi katika kamati ya afya katika kaunti alikiri kwamba changamoto kubwa wanayopitia ni ukosefu wa ardhi mbadala ya kujenga kituo hicho.

“Changamoto kubwa ni kupata hiyo ardhi, lakini hata hivyo tulijadili na tukaona eneo la Mwakirunge linafaa zaidi ingawaje bado hatujapitisha kabisa,” aliongeza mwakilishi huyo.

Shirika la Reach Out Trust liliandaa semina hiyo katika hoteli ya Royal Court mjini Mombasa siku ya Ijumaa ambapo mashirika mbalimbali yalialikwa ikwemo Haki Afrika, wawakilishi kutoka kwa kaunti miongoni mwa mengine.

Semina hiyo ililenga kujadili tatizo la mihadarati katika ukanda wa Pwani kwa ujumla ikiwa ni pamoja na kutafuta suluhu ya tatizo hilo ambapo mashirika hayo yaliahidi kushirikiana pamoja.