Watoza ushuru wawili wa serikali ya kaunti ya Nyamira wanaendelea kuuguza majeraha makali kwenye hospitali ya Kapkatet kule Kericho, baada yao kulumbana na waendeshaji bodaboda wa Mwongori.
Akithibitisha kisa hicho, chifu wa eneo hilo David Ogega alisema kuwa waendeshaji hao bodaboda wenye hasira walikuwa wanapinga kushurutishwa kulipa ushuru wa shillingi mia tatu na maafisa hao, hali iliyosababisha ugomvi kuzuka na kusababisha watoza ushuru wawili kati ya watano kupigwa mawe.
"Ugomvi ulizuka baina ya waendeshaji bodaboda na watosha ushuru hao baada ya maafisa hao kuwashurutisha wanabodaboda hao kulipa ushuru wa shillingi mia tatu kama mapato ya serikali ya kaunti ya Nyamira, na hapo ndipo waendeshaji bodaboda hao wenye hasira walipowapiga mawe watoza ushuru wawili kati ya watano wa eneo la Nyansiongo," alisema Ogega.
Chifu huyo aidha aliwaonya wahusika kujiwasilisha kwa polisi kabla msako mkali haujaanzishwa kuwatia mbaroni.
"Nawaomba wale waliohusika kuwapiga mawe maafisa wa utoza ushuru kujiwasilisha kwa maafisa wa polisi kabla tulazimike kuanzisha msako mkali kuwatia mbaroni washukiwa," alionya Ogega.
Kwa upande wake, katibu wa wanabodaboda wa Mwongori Erick Mokua alipuuza onyo la chifu huyo huku akisena kuwa waendeshaji bodaboda hawako tayari kulipa ushuru hadi pale serikali ya kaunti hiyo itakapokarabati barabara kuu zinazounganisha kituo cha biashara cha Nyaronge na Mwongori.
"Ninavyojua ni kuwa hamna mwanachama wetu aliyewapiga maafisa hao hao na hilo ni jukumu la serikali ya kaunti kuchunguza chunguza, hata hivyo hatuko tayari kulipa ushuru hadi pale serikali ya kaunti itakapokarabati barabara zilizoko katika hali mbaya.