Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Waendeshaji bodaboda katika eneo la Mrima, eneo bunge la Likoni, walifanya maandamano siku ya Jumatatu kulalamikia visa vya kuvamiwa kila mara na kupokonywa pikipiki zao, hasa wanapokuwa kazini nyakati za usiku.

Akizungumza na mwandishi huyu kwa niaba ya wenzake, katika hafla ya mazishi ya mmoja wao aliyeuwawa kwa kukatwakatwa kwa panga siku ya Jumapili, mhudumu mmoja, ambaye hakutaka kutambulika, alisema kuwa wakati umewadia wa maafisa wa usalama kuwajibika kwani visa kama hivyo vya kushambuliwa vimekithiri katika siku za hivi majuzi.

"Siku hizi ukibeba abiria nyakati za usiku huwa una wasiwasi kwa sababu hufahamu kutazuka lipi,” alisema mhudumu huyo.

Aliongeza, "Tunaomba serikali ya kaunti kujali masilahi yetu ya kiusalama kwani nasi tunasaka riziki yetu."

Haya yanajiri siku chache tu baada ya mwendeshaji pikipiki kutoka mtaa wa Mtongwe kupokonywa pikipiki yake na kuuwawa.

Hata hivyo, waendeshaji bodaboda hao ambao waliandamana mpaka maeneo ya Kivuko cha Likoni, walitishia kufanya maandamano makubwa iwapo hatua ya haraka haitachukuliwa.