Waendeshaji bodaboda katika kaunti ya Nyamira wameomba kupewa nambari maalumu ili kurahisisha zoezi la kukusanya ushuru katika kaunti hiyo.
Wahudumu hao walidai kuwa baadhi ya maafisa wa serikali ya kaunti hiyo huonyesha mapendeleo wakati wa kukusanya ushuru.
Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano mjini Kebirigo, waendeshaji bodaboda hao wakiongozwa na mwenyekiti wa kituo cha kebirigo Joshua Mokaya, walisema wanahitaji utaratibu wa kulipa ushuru kuzingatiwa.
Mokaya alisema kuwa hatua hiyo itakuwa njia moja ya kuziba njia za mkato ambazo alisema zimekuwa zikitumiwa na baadhi ya wakusanyaji ushuru kwa kupendelea wahudumu wengine wa bodaboda.
“Tunaomba kila pikipiki isajiliwe kwa ukusanyaji ushuru na tupewe nambari ya kulipa ushuru. Tuliafikia uamuzi huu baada ya kubaini kuwa kuna baadhi ya waendeshaji pikipiki kutoka sehemu fulani ambao wanapendelewa. Wao huruhusiwa kuendelea na biashara yao bila kulipa ushuru,” alisema Mokaya.
Wahudumu hao walisema kuwa waendeshaji bodaboda kutoka sehemu zote za kaunti wanapaswa kuwa na haki sawa bila mapendeleo.