Waendeshaji wa tuktuk mjini Mombasa wamelalamikia sheria mpya zilizotolewa na serikali ya Kaunti inayowapiga marufuku kuingia katikati mwa jiji hilo.
Akizungumza siku ya Jumanne, mwenyekiti wa chama cha waendeshaji tuktuk Obedi Muruli alidai kuwa sheria hizo ni za kuwanyanyasa kwani wateja wao wengi hutaka kusafirishwa hadi ndani ya mji huo.
Aidha, Muruli ameitaka seikali ya kaunti chini ya uongozi wa Gavana Hassan Joho kutafuta njia mbadala ya kuhakikisha kuwa matakwa yao yanazingatiwa na wala sio kutumia nguvu kuwafurusha mjini.
Muruli alisema kuwa wameandaa kufanya maandamano ya amani kwa mara ya pili kwa kuwa licha ya maandamano yao hapo awali na kuitisha mazungumzo baina yao na maafisa wa kaunti, kufikia sasa bado hawajashirikishwa katika mazungumzo hayo.