Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wafanyabiashara katika soko la Kivuko cha Likoni wameitaka serikali ya Kaunti kuwatengezea vibanda vya kudumu na kuimarisha usafi wa soko hilo.

Walisema soko hilo linaendelea kuchakaa kwa sababu ya idara ya kuzoa taka kukosa kuwajibikia kazi yao ya kuhakikisha kuwa taka inaondolewa kila mara kwenye soko hilo.

Wafanyabiashara hao wamelalamikia hali ya usafi pamoja na msongamano wa wahudumu kwenye soko hilo.

Walisema soko linaendelea kumenyeka na kuendelea kupungua kwa kuweko kwa ongezeko la watu ambao wanaingia sokoni kwa ajili ya kutaka kufanya biashara zao.

Walitoa wito kwenye idara ya biashara chini ya Wizara ya Ardhi na mipangilio maalumu ya Kaunti kujaribu na kupanua eneo hilo na kuweka utaratibu mwafaka ambao utahakikisha kuna matumizi bora ya sehemu ambazo zimetengewa wafanyabiashara.

Wakiongozwa siku ya Jumapili na Saidi Athman ambaye ni mmoja wa wanakamati wa wahudumu wa biashara katika soko hilo, walisema kuwa kwa zaidi ya mwaka sasa sehemu hiyo ya soko imeshuhudia kuongezeka kwa wafanyabiashara.

Hali hii, walisema huenda ikaleta mtafaruku miongoni mwa baadhi ya wafanyabiashara akidai kuwa hata kwa sasa kuna wengine wanauza bidhaa zao hata kwenye sehemu ambayo imetengwa mahusus kwa kupita kwa watu na kupitishia mizigo kuingiza na kutoa kwenye soko hilo.

Bw Athman pia alisihi usimamizi wa Kaunti kuratibu mbinu ya kuzoa taka kwenye soko hilo angalau mara tatu au kuwekwe kitovu cha kumwagwa taka hizo kila siku na kuondolewa mwishoni mwa wiki badala ya kurundika kando ya ua wa soko hilo hali ambayo husababisha arufu mbaya kutokana na kuoza kwa taka hiyo.