Huku mvua ikiendelea kunyesha katika sehemu mbalimbali katika Kaunti ya Kisii, wafanyibiashara wa Soko la Daraja Mbili lililoko mjini Kisii wametishia kuandamana kushinikiza seriali ya kaunti kuwajengea vibanda.
Wakiongozwa na Jane Onchiri, wafanyibiashara hao walisema wataandamana kulalamikia hali mbaya ya soko hilo.
Haya yanajiri baada ya wafanyibishara hao kupata hasara siku ya Jumatatu baada ya bidhaa zao kuharibika kufuatia mvua iliyonyesha katika eneo hilo.
Wakizungumza na mwaandishi huyu katika soko hilo, wafanyibiashara hao walitishia kuandamana kuishinika serikali kuwakarabatia soko hilo.
“Tumekuwa tukiomba serikali kutukarabatia soko hili kwa muda mrefu. Sasa tumeamua tutaandamana ili Gavana Ongwae achukue hatua mwafaka,” alisema Cecelia Moraa, mfanybiashara.
Soko la Daraja Mbili ni miongoni mwa masoko makubwa katika Kaunti ya Kisii kwa ubadilishanaji wa biashara baina ya jamii tatu za Kisii, Luo na Maasai pamoja na kujumuisha wafanyibiashara wengine kutoka kaunti zingine.
“Tumekuwa tukisumbuka sana hasa mvua inaponyesha. Leo tumepata hasara kubwa sana maana nguo zetu na nyanya za wafanyibishara wengine zimepotea kufuatia mmonyoko wa udongo,” alisema Victor Ochari, mfanyibiashara.
Aliongeza “Gavana wetu anapaswa kujua kuwa soko hili huipa serikali ya kaunti hela nyingi kupitia ushuru. Tunaomba swala hili lishughulikiwe haraka kabla tuandamane.”