Afisa msimamizi wa usafi mjini Marani, Geoffrey Nyakundi, amewataka wafanyibiashara katika soko la Marani kuboresha mazingira na kuzingatia usafi wanapofanya biashara zao.
Akizungumza siku ya Ijumaa katika soko hilo, Nyakundi aliwaomba wafanyibiashara hao, hasusan wachuuzi wa vyakula, kuhakikisha kwamba wanazingatia usafi wanapofanya biashara zao kwa kutotupa uchafu ovyo.
Afisa huyo alisema kuwa kuna sehemu mbalimbali za kutupa taka katika soko hilo, na kuna haja ya kila mfanyibiashara kuhakikisha kwamba anatupa taka katika maeneo hayo yaliyotengwa baada ya kufagia.
“Naomba wanaonunua vyakula kutoka kwa wachuuzi kupiga ripoti kwetu kuhusu wachuuzi wasiozingatia usafi ili tuchukue hatu ya kisheria kwa mchuuzi husika,” alisema Nyakundi.
Wakati huo huo, afisa huyo aliwataka wafanyibiashara kuwa na pipa la kutupa taka, kama njia moja ya kuhakikisha usafi wa mji na kujikinga kutokana na magonjwa mbalimbali yanasababishwa na uchafu, kama vile kipindupindu na mengine mengi ambayo ni hatari kwa maisha ya binadamu.