Wafanyibiashara katika Soko la Kongowea wanahofia usalama wao kutokana na kisa kimoja ambapo majambazi wawili waliokuwa wamejihami na bunduki walivamia gari la manispaa lililokuwa limetoka kuchukua ushuru kutoka soko hilo.
Wakizungumza siku ya Ijumaa, wafanyibiashara hao walisema kuwa wanahitaji usalama wa kutosha sokoni humo ili kuepeuka uvamizi zaidi kutokea.
Wakiongozwa na Tommy Simba, ambaye ni mfanyibiashara wa viazi, walisema kuwa soko hilo hutengeneza zaidi ya shilingi milioni moja kwa siku na kusisitiza kuwa iwapo usalama hautaimarishwa, basi kuna uwezekano wa kupoteza pesa hizo kwa vile wezi watagundua kuwa hakuna usalama wa kutosha sokoni humo.
“Tunaitaka idara ya usalama katika Kaunti ya Mombasa kuweka maafisa wa polisi wakutosha katika kila lango la soko hili wa kuwakagua watu wanaoingia sokoni,” alisema Simba.
Haya yanajiri baada ya wezi kuiba Sh200,000 na kujeruhi Tolbert Ochieng, dereva wa gari lilokuwa likisafirisha pesa hizo.
Afisa mkuu wa Kitengo cha usalama katika Kaunti ya Mombasa Charles Karisa, alisema kuwa uchunguzi utafanyika ili kuwatambua waliotekeleza wizi huo na hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.