Wafanyibiashara katika soko la Kongowea mjini Mombasa wamelalamikia mirundiko ya uchafu katika soko hilo hali ambayo imewatia hofu hasua wakati huu ambapo wageni wanazuru mjini humo.
Akiongea na wanahabari katika soko hilo, katibu wa chama cha wafanyibiashara katika soko hilo Peter Nyaga amesema kwamba mirundiko hiyo ya takataka katika soko hilo imeshuhudiwa kwa muda mrefu licha ya wao kuropti kwa wahusika kukusanya taka hizo.
Nyaga alisema kwamba iwapo soko hilo litaendelea kusalia na taka hizo, basi huenda ikasababisha madhara ya kiafya na hata kufungwa kwake na maafisa wa afya.
Nyaga alidokeza kuwa licha ya biashara katika soko hilo kunoga kufuatia kuongezeka kwa wageni na watalii wanaozuru Mombasa, Nyaga aliirai serikali ya kaunti ya Mombasa kupitia kwa wizara ya biashara kuwajibikia majukumu yao kikamilifu na kulinusuru soko hilo.
“Tunawaomba wahusika kulichukulia swala hilo kwa dharura na kulisafisha soko letu ili kuwa na mazingira bora na kuwavutia wateja wengi zaidi kwani soko hili linaunganisha baishara ya nchi za Afrika Mashariki”, alisema Nyaga.
Soko hilo linalohudumia wafanyibiashara kutoka Afrika masharika wameanza kuhofia kudidimia kwa biashara ndani na nje ya soko hilo iwapo mazingira bora hayataidhinishwa.