Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wafanyabiashara katika soko la Kibuye jijini Kisumu, wamelalamikia kile wanachosema ni hatua ya maafisa wa idara ya kuzoa taka katika kaunti ya Kisumu, kujikokota kuondoa taka sokoni humo.

Walisema kuwa taka hizo ambazo zimerundikana kwenye maeneo mbali mbali ya soko hilo, zinatoa uvundo kiasi cha kuyumbisha biashara zao.

Walitaka taka hizo kuondolewa haraka iwezekanavyo, wakisema kuwa uwepo wa taka kwenye soko hilo unaathiri pakubwa biashara zao.

Walisema kuwa Kibuye ni soko kubwa na lina uchafu mwingi, wakisisitiza kuhusu umuhimu wa taka kuondolewa sokoni humo kila siku, na sio baada ya siku mbili jinsi inavyofanyika sasa.

Aidha, waliitaka serikali ya kaunti ya Kisumu kuwajengea vibanda kwenye soko hilo, ili kuwawezesha kujikinga wakati wa jua kali na mvua.

“Tunahitaji vibanda kwenye soko hili kwa sababu tunaumia sana wakati kama huu wa jua kali. Hivi karibuni tutahaingaika hata zaidi kutokana na mvua ambayo inatarajiwa kuanza kunyesha wakati wowote,” alisema Elizabeth Akinyi, ambaye ni mmoja wa wafanyabiashara katika soko hilo.

Hata hivyo, wafanyabiashara hao waliipongeza serikali ya kaunti ya Kisumu kwa kuweka taa kwenye soko hilo na kwenye mitaa mbali mbali jijini Kisumu, hali ambayo imechangia kuimarika kwa usalama.

Soko la Kibuye liko mkabala wa makao makuu ya Kanisa Katoliki nchini jimbo Kisumu, kwenye barabara kuu ya Kisumu – Kakamega.

Soko hilo huwakutanisha wafanyabiashara kutoka maeneo mbali mbali ya Magharibi ya Kenya kila siku.