Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Chama cha kutetea maslahi ya wafanyikazi wa serikali za kaunti KCGWU tawi la Nyamira, kimelalamikia hatua ya bunge la kaunti kutowapa majukumu wafanyikazi waliokuwa wakifanya kazi na manispaa ya Nyamira hapo awali.

Akiwahutubia wanahabari mjini Nyamira siku ya Ijumaa, katibu mkuu wa chama hicho tawi la Nyamira Patrick Mobegi, alisema kuwa bunge la kaunti hiyo lina mipango yakuajiri wafanyikazi wapya ilhali wafanyikazi wa manispaa iliyokuwemo kabla ya serikali za ugatuzi kuanza kazi hawajapewa majukumu, kinyume na ilivyo kikatiba.

"Tunafahamu kuwa bunge la kaunti hili lina mipango yakuajiri watu wanaowapendelea ilhali wafanyikazi ambao wamekuwa wakifanya kazi na serikali za manispaa hawajapewa majukumu licha ya kupokea mishahara kwa mwaka wa tatu sasa," alisema Mobegi.

Mobegi aidha aliuliza ni kwa nini bunge la kaunti hiyo linataka kuwahamisha wafanyikazi hao hadi kwa afisi ya gavana, akisema hiyo ni mbinu ya bunge hilo kuwaajiri watu wanaowapendelea.

"Bunge hili lina mipango yakuhamisha wanachama wetu hadi kwa afisi ya gavana ili kufanya kazi pale. Kwanini wafanyikazi hao wafanye kazi chini ya afisi ya gavana huku kukiwa na majukumu mbalimbali yakufanywa bungeni? Chama chetu kamwe hakitakubaliana na hatua hiyo,” alisema Mobegi.