Zaidi ya wafanyikazi 250 wa kampuni ya kusambaza maji mjini Nakuru Nawassco, Jumanne walifanya maandamano ya amani nje ya makao makuu ya kampuni hiyo mjini Nakuru, na kudhihirisha walichoita ‘kumuunga mkono’ meneja wao bwana James Ng’ang’a.
Huku wakibeba mabango, wafanyikazi hao waliapa kutorejea katika maeneo yao ya kazi, hadi hoja iliyowasilishwa mahakamani dhidi ya Ng’ang’a iondolewe.
Walimlaumu meneja mkurugenzi wa awali wa Nawassco bwana Geoffrey Asanyo kwa kumwandama kichini chini mkurugenzi wa sasa, kutokana na kufaulu kwa kampuni hiyo chini ya uongozi wake.
Wakiongozwa na Francis Makokha na Zephania Nyambane waliozungumza na wanahabari kabla ya kufanya maandamano hayo hadi katika mahakama za Nakuru, wafanyikazi hao walisema, “Nawassco imeonyesha rekodi nzuri za utendakazi tangia bwana Ng’ang’a achukue hatamu za uongozi kama meneja mkurugenzi.”
Wafanyikazi hao walikita kambi katika mahakama za Nakuru, ambapo hoja imewasilishwa na shirika moja la kutetea haki za kibinadamu, kuchangamoto kuchaguliwa kwa mameneja wawili wa kampuni hiyo, na waliondoka baada ya takriban saa tatu.
Waliotajwa na shirika hilo (Trusted Society Alliance Of Human Rights, TSAHR) kupitia kampuni ya mawakili ya Gitobu Imanyara, ni pamoja na NAWASSCO, bwana Ng’ang’a na serikali ya kaunti ya Nakuru.
Kesi hiyo haikuendelea kwa kuwa jaji Maureen Odero hakuwa mahakamani, ikibainika kwamba alikuwa na majukumu mengine nje ya Nakuru.