Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Zaidi ya wafanyikazi 800 kutoka shamba la Alphega linalomilikiwa na Seneta wa Baringo Gideon Moi waliandamana Jumanne jioni kilomita 9 hadi eneo la Mogotio wakilalamikia uongozi mbaya na kucheleweshwa kwa mishahara yao kwa muda wa miezi miwili sasa.

Wakibeba matawi na mabango walisema kuwa, Seneta Gideon Moi anashughulika na siasa za Kericho kwa kuahidi uongozi mzuri, lakini amesahau na kutelekeza wafanyikazi wake.

Wakiomba kubanwa majina yao kwa misingi ya kudhulumiwa kazini, walisema hawajapokea mishahara yao ya mwezi January na Februari.

“Tangia Januari hadi wa sasa hatujapata mishahara yetu, na badala ya kuja kutuletea pesa, seneta Gideo ndiye huyo tunamuona kwa siasa za Kericho. Kama anataka uongozi wa taifa, aanze na nyumbani ashibishe wafanyikazi wake kwanza” akasema mkaazi mmoja.

Walidokeza kuwa, wamekuwa wakinyanyaswa licha ya kufanya kazi nzito kwenye shamba hilo la mkonge, na kuwa na familia zinazowategemea. Walitaka kuandamana hadi kabarak nyumbani kwa rais mstaafu Moi, kumwomba azungumze na kijana wake awape haki yao ya mshahara.

“Tuna watoto wanaoenda shuleni, na wanamahitaji. Familia zetu zinataka kula, kunywa na kukaa vizuri. Aachane na siasa kwanza atupe haki yetu ambayo tumefanyia kazi” akasema mkaazi mwingine.

Hata hivyo maandamano hayo yalitulizwa na msaidizi wa senata Gideon Moi, Robert Muigai aliyekumbwa na wakati mgumu kwani wafanyikazi hao walikuwa wamekataa kuhutubiwa naye.

Ni baada ya makubaliano kwamba watapata mshahara wa mwezi Januari kufikia Ijumaa tarehe 4, Machi 2016, na baada ya siku zingine nne wapate mshahara wa mwezi Februari.