Wafanyikazi wa mamlaka ya maendeleo Pwani CDA siku ya Jumatano walifanya mgomo na kususia kuendelea na kazi kwa madai ya kunyanyaswa na mwajiri wao.
Wafanyikazi hao wapatao 400 walikusanyika nje ya ofisi za mamlaka hiyo wakiwa wamebeba mabango yaliyooandikwa ujumbe unaoashiria kilio chao cha kutaka mkurugenzi wa mamlaka hiyo kuondolewa.
Wakiongea na mwandishi huyu nje ya ofisi hizo, wafanyikazi hao wakiongozwa na Fatuma Daba walisema kuwa kwa kipindi cha miezi 4 hawajalipwa mishahara yao huku usimamizi wa shirika hilo ukikosa kutoa maelezo yoyote.
“Hatujalipwa mishahara yetu kufikia sasa, tuliwasilisha lalama zetu kwa mkuu wa mamlaka lakini anatupuuza, hali hiyo imetuingiza katika hali ngumu sana ya maisha,” alisema Fatuma.
Mbali na mshahara, aidha wafanyikazi hao pia wanasema kuwa mamlaka hiyo ilikuwa ikikwepa kuwalipa pesa maalum ambazo wanafaa kulipwa wakati wanapoenda likizo.
Mnamo tarehe 6 Januari wafanyikazi hao walipeana siku 14 kwa mamlaka hiyo kushughulikia maslahi yao kabla ya kufanya mgomo.
Ni baada ya siku hizo kuisha ndipo wakaamua kufanya mgomo huo huku wakishinikiza mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo James Mangi kuondolewa na kuletewa mtu mwingine ambaye atayaghulikia matatizo ambayo yamekuwa yakiwakumba.
“Huyu mkuu wa hapa yuko na kundi la watu wachache ambao anafanya nao kazi kwa karibu huku akipuuza wengine, sisi tunataka aondolewe pamoja na hao wenzake kwa sababu hata tukilipwa bado matatizo ni haya tu,” aliongeza Dahir kone, mmoja wa wafanyikazi.
Wakati huo huo wameongeza kusema kuwa wengi wao wameshindwa kulipa kodi za nyumba pamoja na kutekeleza majukumu mengine ambayo ni kulipia watoto karo ya shuleni miongoni mwa zingine.
Mamlaka ya maendeleo Pwani ni moja kati ya mamlaka 6 zilizoanzishwa humu nchini kwa lengo la kufuatilia na kutekeleza miradi ya kimaendeleo inayoendeshwa kwa wananchi.