Maafisaa wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi EACC kutoka Nakuru walivamia makaazi ya mafisaa wawili wakuu katika serikali ya kaunti ya Nakuru Jumatano.
Wakiongozwa na afisaa wa tume hiyo Sadat Lunani, maafisa hao wamesema walifanya msako katika nyumba ya kaimu waziri wa fedha wa kaunti ya Nakuru Anne Njenga pamoja na nyumba ya afisa mwandamizi na mhasibu mkuu wa kifedha Billy Chemirmir kutokana na madai ya ufisadi.
Kwa mujibu wa lunani wawili hao wanasemekana kuwa na mali ambayo haieleweki waliipata vipi, ambayo thamani yake ni zaidi ya shilingi milioni 20.
Wawili hao aidha wameachiliwa lakini watahitajika kufika katika afisi za tume hiyo zilizo mjini Nakuru wakati wowote watakapohitajika kufika mbele ya tume hiyo.
Haya yanajiri siku chache baada ya gavana wa kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua kuonya wafanyikazi wa kaunti kutojihusisha na ufisadi.