Share news tips with us here at Hivisasa

Mashirika mbalimbali ya kijamii yamejitokeza kuwahamasisha wafungwa Pwani kuhusu ugonjwa wa ukimwi, kama njia moja ya kukabiliana na maambukizi mapya na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo katika magereza.

Mashirika hayo yakiongozwa na Shirika la kupambana na utumizi wa mihadarati eneo la Pwani ‘Reach out Centre Trust’, yameendeleza hamasa hizo kuhusu ugonjwa wa ukimwi kwa wafungwa wa Gereza la Shimo la Tewa na Kwale, pamoja na kuwapima virusi kwa hiari.

Hamasa hizi zimetolewa ili kuwawezesha wafungwa hao kufahamu hali zao za HIV na jinsi ya kujikinga ili kuepukana na maambukizi ya virusi vya ukimwi magerezani.

Katika mahojiano na mwanahabari huyu katika gereza la wanaume la mjini Mombasa siku ya Ijumaa, mwanaharakati wa kupambana na utumizi wa dawa za kulevya kutoka shirika la Reach out Centre Trust, Saria Goga, alisema kuwa hamasa hizo zitawasaidia wafungwa hao kujikinga na maradhi ya kiafya.

Mbali na kuwapima virusi vinavyosababisha ukimwi, Goga alisema kuwa wanawashauri wafungwa walioathirika na utumizi wa dawa za kulevya kuhusu namna ya kujinasua baada ya kumaliza vifungo vyao.

“Tumeonelea kuchukua jukumu la kutembelea magereza yetu na kuwasaidia ndugu zetu kufahamu hali zao za kifya kwa kuwapa hamasa na kuwashauri kipimwa kwa hiari, ili kuona kwamba wanajikinga na maambukizi ya virusi vya ukimwi,” alisema Goga.

Hata hivyo ameshinikiza kuwepo kwa ushirikiano mwema baina ya wafungwa hao na maaskari wa gereza ili kuwasaidia kuboresha mazingira bora na afya.