Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwalimu mkuu wa Shule ya upili ya wavulana ya Nyambaria, iliyoko Kitutu Masaba, Kaunti ya Nyamira, ameomba wasamaria wema kuwasaidia kukarabati paa zilzoharibiwa na mvua.

Akiwahutubia wanahabari shuleni humo, Robinson Mokaya alisema kuwa paa za madarasa tatu ziliharibika kutokana na upepo mkali uliosababishwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika eneo hilo.

"Kuna paa za madarasa tatu zilizongolewa na upepo mkali uliosababishwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha, hali ambayo imetuathiri pakubwa," alisema Mokaya.

Mokaya amewaomba wahisani kujitokeza kuisaidia shule hiyo kuezeka upya paa zilizoharibika.

Alisema kuwa itakuwa vigumu kurejelea shughuli za kawaida shuleni humo mapema mwakani shule zitakapofunguliwa kwa muhula wa kwanza, paa hizo zisipokarabatiwa.

"Nawaomba wahisani hasa serikali ya Kaunti ya Nyamira ijitokeze kutusaidia kuezeka upya paa zilizoanguka kwa kuwa itatuwia vigumu kurejelea shughuli za kawaida shule zitakapofunguliwa mwezi ujao," alisema Mokaya.