Wahudumu wa mashirika saba ya magari ya kubeba abiria kutoka Naivasha hadi Nakuru, waliandamana Ijumaa Machi 11, 2016 wakilaumu kampuni ya Molo Group kwa madai ya kugawanya watu wa Naivasha, na kusababisha mtafaruku wa abiria.
Maandamano hayo yalikwamisha shughuli kwenye uwanja wa matatu za Nakuru mjini Naivasha na yalihusisha mashirika ya Nagil, NNUS, 4-NTE, Soko Huru, Mololine, Nyamakima na Crossland.
Molo Group inalaumiwa na mashirika hayo “kwa kuhonga manispaa ya mji wa Naivasha” ili kuruhusiwa kubebea abiria wanaoelekea Nakuru katika uwanja wa matatu za Kinangop.
Aidha maandamano hayo yalihusisha wauzaji wote wa maduka na vioski kwenye uwanja wa Nakuru mjini Naivasha.
Kulingana na msimamizi wa nidhamu kwenye uwanja huo wa matatu za Nakuru mjini Naivasha bwana Njehia Kamau, tayari Molo Group imetengewa pahali pa kubebea abiria katika eneo hilo, lakini wanatafuta eneo la pili jambo ambalo alisema “ni dhulma na ubinafsi wa kusababisha vita mjini Naivasha.”
Hata hivyo Base Commander wa Naivasha Hellen Nzevu na maafisa wake waliharakisha kutatua maandamano hayo kabla ya kuzua utata na kuamrisha Molo Group kutobebea abiria uwanja wa Kinangop tena.