Huku wanafunzi pamoja na wasafiri kutoka maeneo mbali mbali katika Kaunti ya Mombasa wakilalamikia kupanda kwa nauli, baadhi ya wahudumu wa magari ya usafiri wamejitokeza na kukana madai hayo na kusema kuwa si wote wameongeza nauli.
Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumanne katika eneo la Makupa katika Kaunti ya Mombasa, mwenyekiti wa matatu ya MOM Sacco Abed Ramah alisema kuwa baadhi ya magari hayajapandisha bei ya kusafiri vile inavyodaiwa na wengi wa wasafiri wa msimu huu wa kurudi katika shule.
Ramah alisema japokuwa kila mtu ana haki ya kufanya anavyotaka, lakini kuna wale wanachukua nafasi hiyo kujifaidi na kujitajirisha kinyume na sheria na utaratibu unasimamia huduma za barabarani na kinyume na wizara ya uchukuzi.
Alidai kuwa mengi ya magari yaliyo kwenye chama chao hayajaongeza bei na yanatumia ada za kawaida, na hufanya hivyo wakati inabidi hususan nyakati mafuta yamepandishwa bei na halmashauri ya kudhibiti kawi na mafuta nchini.
“Sacco yetu bado tunadumisha ile ada ya kawaida na hatupandishi nauli bila sababu, ila tu wakati bei ya mafuta imefanya kuenda juu au kuongezwa na halmashauri husika hivyo basi wale wanafanya hivyo hukiuka utaratibu wa kudhibiti masuala ya usafiri na uchukuzi, ” alidai Ramah.