Biashara katika barabara ya Mosque mjini Nakuru nusra zisimame wakati wahudumu wa Tuk tuk walirushiana makonde sababu kuu ikiwa ni mteja.
Wahudumu hao wanne walikua wamemtegea mteja mmoja ambaye alikua akitoka kwenye hoteli ya Carnation, na punde tu wakati mteja huyo alipotoka hotelini, wanne hao walianza kumng'ang'nia na baadaye ikawa vita vilivyo dumu kama dakika thelathini huku raia wakishangilia.
Kulingana na Simon Waithaka, aliyeshuhudia vita hivyo, mhudumu mmoja wa Tuk tuk alikua ameongea na mteja huyo kuwa angeenda kumchukua katika hoteli hiyo, lakini kwa sababu ya biashara kuwa chini, wenzake walimfuata ili kumnyang'anya mteja wake na hapo ndipo vita vilizuka.
"Kuna jamaa ambaye alikua ameambiwa amkujie mteja flani kwa hii hoteli, lakini kwa sababu biashara haikuwa mzuri siku nzima, hawa wengine walitaka kumnyang'anya mwenzao mteja na hapo ndipo vita vilianza," alisema Waithaka, ambaye ni mfanyakazi wa duka la jumla la Flamco.
Baadaye wahudumu hao waliweza kutiwa mbaroni na polisi waliokuwa wakishika doria kwenya barabara ya Mosque na kuwapeleka katika kituo kikuu cha polisi cha Nakuru.