Aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi Ann Waiguru amesema kuwa maisha yake yamo hatarini na anahitaji maafisa wa polisi kumpa ulinzi.
Kwenye barua aliyomwandikia Inspekta Jenerali Joseph Boinnet, Bi Waiguru alisema kuwa amepokea vitisho kutoka kwa wanasiasa wakuu, na pia matamshi yanayotolewa na kiongozi wa walio wengi bungeni Aden Duale na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen yanahatarisha maisha yake.
“Tukizingatia majira ya siasa humu nchini kwa sasa, pamoja na matamshi yanayotolewa na wanasiasa hawa, nahisi kwamba maisha yangu yamo hatarini,” alisema Waiguru kupitia kwa barua aliyomwandikia Boinnet.
Waiguru pia alihusisha vitisho hivyo na hati yake ya kiapo aliyoitoa mahakamani ambapo aliwataja wanasiasa wakuu kuhusika na ubadhirifu wa fedha katika sakata ya NYS.
Waiguru aidha alisema kuwa usemi wa baadhi ya viongozi kuwa ana nia ya kuutawanya mrengo wa Jubilee ni ya uwongo.
“Baadhi ya wanasiasa wakuu wamedai kuwa mimi nanuia kuuvunja mrengo tawala wa Jubilee,” aliongeza Waiguru.
Waiguru aidha amesalia na msimamo kuwa aliondolewa mashtaka na Tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC hadi pale mmoja wa washukiwa wakuu kwenye sakata hiyo alimtaja tena kuhusika katika sakata hiyo, madai ambayo Waiguru alisema ni njama ya wahusika wakuu kwenye sakata hiyo.
“Naamini mashirika ya kufanya uchunguzi lakini nahisi kuwa kutakuwepo na jaribio la kuathiri uchunguzi huo. Nahisi kwamba nisipopewa ulinzi wa kutosha, nitakuwa nahatarisha maisha yangu,” aliongeza Waiguru.
Akidhibitisha kuwepo kwa barua hiyo, msemaji wa huduma za polisi nchini NPS Bw George Kinoti alisema kuwa walipokea barua kutoka kwa Bi Waiguru bali kwa sasa uamuzi ama hatua yoyote haiwezi chukuliwa.