Zaidi ya vitambulisho 11,000 vya kitaifa vimesalia katika afisi za usajili wa watu katika Kaunti ya Kisumu, kufuatia wenyewe kukosa kuvichukua.
Akizungumza siku ya Jumanne, Kamishna wa Kaunti ya Kisumu John Elungata alitoa wito kwa yeyote aliyejiandikisha kuchukua kitambulisho cha kitaifa Kisumu kufika katika afisi husika kuchukua stakabadhi hiyo muhimu ya kitaifa.
Elungata vile vile alitoa wito kwa wazazi ambao watoto wao wamehitimu umri wa miaka 18 na walijisajili kuchukua vitambulisho vya kitaifa ilhali wako maeneo ya mbali, wafike katika afisi za serikali za usajili kuwachukulia wanao vitambulisho hivyo.
Kamishna huyo alisema kuwa hivi karibuni maafisa wa polisi wataandaa msako wa kuwatafuta watu ambao wametimu umri wa miaka 18, ilhali hawana vitambulisho vya kitaifa.
Elungata alisikitikia hali ya watu kukosa kufika katika afisi za machifu na manaibu wao kuchukua vitambulisho vyao, na kusema kuwa vitambulisho hivyo vilipelekwa katika afisi za maafisa hao wa utawala ili kuwafikia wenyewe kwa urahisi.
Kamishna huyo ametoa wito kwa wale waliotuma maombi ya kupewa vitambulisho kufika kwenye afisi za utawala au kwenye afisi za usajili wa watu ili kuchukua stakabadhi hizo.