Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakaazi wa Likoni, Kaunti ya Mombasa wamesema wanashangazwa na kimya cha mbunge wa eneo hilo Masoud Mwahima, kuhusu swala la Shamba la Waitiki linaloendelea kuzua utata.

Licha ya kwamba Rais Uhuru Kenyatta alizuru eneo hilo mapema mwaka huu na kutoa hati miliki kwa maskwota hao, viongozi wa kisiasa katika ukanda wa Pwani wameonekana kutilia siasa swala hilo tata huku wakaazi wakibaki katika njia panda.

Viongozi mbalimbali wamekuwa wakiwasisitizia maskwota hao kutolipa ada ya shilingi elfu 182 waliyoagizwa na serikali kulipa, mmoja akiwa ni Gavana wa Mombasa Hassan Joho aliyetoa matamshi hayo alipozuru eneo hilo wiki chache zilizopita.

Hata hivyo mbunge wa eneo hilo Masoud Mwahima amekuwa kimya kuhusu swala hilo huku wakaazi hao wakiwa na hamu ya kutaka kujua usemi wake ni upi.

“Mbunge wa hapa amenyaza kimya tangu wakati wa ile hafla ya rais. Tumesikia gavana akisema tusilipe pesa hizo, serikali nayo bado inasisitiza tulipe. Sasa tumeshindwa kuelewa kwanini swala kama hili litiliwe siasa,” alisema mkaazai mmoja.

Mwahima hajaonekana tena hadharani tangu wakati huo na sasa wakaazi hao wanataka kumskia akiongea na kutoa muelekeo mwafaka kwao, kwani wengi wao wameshindwa kuelewa njama inayoendelea kuhusu shamba hilo.

Sasa wakaazi hao wanaishi na wasiwasi licha ya kupewa hati miliki hizo, huku wakitilia shaka mgawanyiko uliopo miongoni mwa viongozi wa eneo hilo kisiasa.

Siku ya Jumatatu mshirikishi mkuu wa usalama katika ukanda wa Pwani Nelson Marwa aliwaonya wanasiasa wanaoendelea kupiga siasa kuhusu shamba hilo, akisema kuwa hatua hiyo inazidi kurudisha nyuma maendeleo.

Wakati wa kutoa hatimiliki hizo, Rais Kenyatta aliwaambia maskwota hao kwamba lazima walipe ada ya shamba hilo ya shilingi elfu 1 kila mwezi, hadi pale watakapokamilisha shilingi elfu 182 zinazohitajika.