Maafisa wa utawala wametakiwa kuwahimiza wananchi kuchukua vitambulisho vya taifa ili wapate kusajiliwa kama wapiga kura kwenye zoezi la usajili linaloendelea.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa katika mkutano wa hamasa kwa jamii, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Haki Afrika, Hussein Khalid, alisema kwamba vitambulisho vingi bado vingali katika afisi za usajili wa watu na zile za machifu.
Mwanaharakati huyo wa haki za binadamu alielezea haja ya wale ambao hawajachukua vitambulisho vyao kufika katika afisi hizo kuvichukua kabla ya muda wa usajili kukamilika mwezi ujao.
“Tunawaomba wakaazi tafadhili jitokezeni mchukue vitambulisho vyenu vya kitaifa kwa sababu zaidi ya vitambulisho 27, 900 bado havijachukuliwa na idadi hiyo ni kubwa mno katika Kaunti ya Mombasa,” alisema Khalid.
Kauli yake hii inajiri baada ya Afisa Mkuu wa Usajili wa Watu eneo la Pwani Aggrey Masai kuwahimiza wakazi wa eneo hilo kuchukua vitambulisho vyao.