Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Baadhi ya wakaazi Mombasa wamepinga hatua ya kubadilishwa kwa jina ya barabara ya Nyali na kupewa jina jipya la Fidel Odinga, kwa makumbusho ya mtoto wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatano, muda mchache tu baada ya barabara hiyo kuzinduliwa, Rophas Murabua, mkaazi, alidai kuwa, kubadilishwa jina la barabara hiyo, ni njia ya kujipatia sifa na umaarufu wa kisiasa hasa kwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Murabua aliongeza kuwa haoni umuhimu wowote wa barabara hiyo kubadilishwa jina ikizingatiwa kuwa watu wengi wanaitambua kama barabara ya Nyali.

Hamisi Saidi, mkaazi wa Kongowea, alisema kuwa mkoa wa Pwani una viongozi mashuhuri ambao pia wanahitaji kutajwa, ili kuwa ukumbusho kwa jamii za eneo la Pwani.

Aidha, aliuliza ni kwanini viongozi wa Pwani hawatajwi kwenye barabara za kaunti nyinginezo nchini.

Kauli hii inajiri baada ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga kushuhudia kufunguliwa kwa barabara hiyo iliyopewa jina la mwanawe marehemu Fidel Odinga.