Wakaazi wa eneo la Pwani wameshauriwa kutokubali kulaghaiwa na kujisali maeneo ambayo baadhi ya wanasiasa wanatoka ili kuwachagua wakatia wa uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Kiongozi wa vijana katika eneo la Kisauni, Kaunti ya Mombasa Maxwell Masai alisema kuwa hatua hiyo inalenga kuwakandamiza wakaazi kwani lengo kuu la viongozi kama hao ni kujinufaisha binafsi wala hawana azma ya kuwasaidia Wakenya.
Masai alisema kuwa jukumu la wananchi ni kutumia kura yao vyema na kuwachagua viongozi waadilifu walio na malengo ya kubadili sura ya eneo la Pwani katika masuala ya maendeleo na wala sio kujinufaisha binafsi.
Kiongozi huyo wa vijana amewataka wakaazi hao kujitokeza kwa wingi na kujisajili kama wapiga kura, ili kuwabandua madarakani viongozi wabinafsi, wafisadi na wanyanyasaji, na kubadilisha uongozi uliyopo kwa sasa, ili kuona kuwa wakaazi wanafaidika kimaendeleo.
“Tunawaomba wakaazi kuwa waangalifu na baadhi ya viongozi kama hao kwa sababu ndio watakaofanya eneo hili kuwa nyuma kimaendeleo na hata kidemokrasia. Wakazi wanapaswa kuhakikisha kuwa hawadanganywi na viongozi hao walafi,” alisema Masai.
Kwa sasa mchakato wa kisiasa unaendelea katika eneo nzima la Pwani huku wakaazi wakishauriwa kujitokeza kwa wingi na kujisajili kama wapiga kura ili kujihusisha moja kwa moja katika uchaguzi mkuu ujao.