Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Huku Idara ya Usalama katika eneo la Pwani ikendelea kukabili makundi haramu ya vijana, bado wakaazi wanaendelea kulalamikia kudorora kwa usalama katika baadhi ya mitaa Mombasa.

Wakaazi wa mtaa wa Majengo King’orani, Kaunti ya Mombasa, wamesema kwamba bado kuna vijana wanaowavamia wapita njia nyakati za usiku na kuwapora mali yao.

Wakiongea na mwandishi huyu siku ya Jumapili mjini humo, wakaazi hao waliitaka idara ya usalama kuwakabili vijana hao ambao wameharibia mtaa huo sifa, huku hofu ikitanda kila usiku.

“Huu mtaa unaogopewa sana kutokana na vijana hao ambao hutembea na visu pamoja na panga, huku wakisimamisha wapita njia na kuwapora pesa na simu,” alisema mkaazi mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina.

Inasemekana kwamba vijana hao ni wa umri mdogo wa kati ya miaka 20 na 26, huku pia kukiwa na madai kwamba wanalenga sana wageni ambao ni mara yao ya kwanza kupitia katika mitaa hiyo.

“Vijana hao huzurura kwenye njia za vichochoro na kuwatishia na kuwavamia wageni,” aliongezea mkaazi huyo.

Mama mmoja anayefanya biashara ya kuuza chakula alisema kwamba alivamiwa siku ya Jumamosi alipokuwa akitoka kazini na kusalimisha simu yake kwa vijana hao ili kujinusuru.

“Nilishambuliwa na vijana wawili walionionyesha visu, ikabidi nimewapa simu yangu. Hatahivyo, hawakupata pesa kwa sababu nilikuwa nimezificha mbali,” Alisema mfanyibiashara huyo.