Afisa mkuu wa afya kaunti ya Nakuru Samuel King’ori amewatolea wakaazi wa kaunti hiyo changamoto ya kuchoma wafu wao kutokana na uhaba wa nafasi kwenye makaburi ya umma.
King’ori alisema kwamba kaburi la Kaskazini mwa Nakuru na lile la Naivasha mjini tayari yamejaa huku makaburi mengine yanayosalia katika kaunti hiyo yakitarajiwa kujaa kufikia mwishoni mwa mwaka 2016.
Akiongea ofisini mwake Alhamisi, Kingori alisema: “Kaunti ya Nakuru imeishiwa na nafasi za kuzika wafu. Eneo la North cemetery limejaa, sawia na kaburi la Naivasha.”
Alisema kaunti hiyo ilitoa ilani ambayo inaipa ofisi yake mamlaka ya kufunga makaburi yaliyojaa, na kupiga faini ya Ksh 1,500 wale wanaoendelea kuzika watu kwenye makaburi hayo.
“Kaunti ilitoa ilani kuhusiana na hilo Juni 2, 2015 kulingana na sheria za afya ya umma,” Kingori alisema.
Hata hivyo alikiri kwamba Nakuru imekuwa ikikabiliwa na matatizo ya kupata ardhi ya makaburi.
“Watu wengi wanahofia kutuuzia ardhi kwa sababu hawataki kukaa karibu na makaburi ama ardhi yao kupakana na makaburi,” alisema.
Kulingana na sheria ardhi ya makaburi, lazima mchanga wake uwe na uwezo wa kuruhusu kuoza haraka kwa miili inayozikwa humo, na lazima pia ifanyiwe ukaguzi na mamlaka ya kutunza mazingira nchini, NEMA.
Hata hivyo ikizingatiwa kwamba kaunti ya Nakuru husheheni watu wa tabaka, dini na imani tofauti, huenda wazo la kuchoma miili ya wanaokufa likapata upinzani mkali.