Share news tips with us here at Hivisasa

Wakaazi wa Pwani wamehimizwa kujitokeza na kuvitembelea vituo vya afya ili kujua hali zao kutokana na kukithiri kwa maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Shirika la kijamii la Jamii Imara limesema kwamba idadi kubwa ya vijana ndio huambukizwa virusi hivyo kutokana na kujihusisha na ngono za kiholela bila ya kutumia kinga licha ya kufahamu athari za ugonjwa huo.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumapili baada ya warsha ya hamasisho kuhusu mbinu za kujikinga na maradhi ya virusi vya Ukimwi, afisa mkuu wa shirika hilo Joy Rui alisema kwamba maeneo ya Likoni, Malindi, Mombasa na Watamu yameorodhesha idadi kubwa ya waathiriwa wa maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Rui alisema kuwa hali hiyo imechangiwa na starahe nyingi ambazo vijana wanajihusisha nazo, na kusema kuwa lazima hamasa kuhusu athari za virusi hivyo kufanywa kwa jamii hadi mashinani ili kuwaepusha na ugonjwa huo

Alisisitiza kuwa njia mwafaka ya kujikinga kutokana na virusi hivyo ni kutumia mipira ya kondomu.

“Tumeona idadi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi ikiongezeka hapa Pwani na ni kutokana na vijana wengi kutolichukulia kwa umuhimu swala la kuzuru vituo vya afya kutambua hali zao,” alisema Rui.

Rui alisema kuwa shirika hilo litaendeleza hamasa mashinani na kuwalenga zaidi vijana na akina mama wajawazito, ili kuona kwamba wanajitenga na ngono za kiholela ambazo zimepelekea kuongezeka kwa maambukizi ya virusi.