Ili kukabiliana na dhuluma za kijinsia haswa unajisi dhidi wa wanawake, mwakilishi mmoja wa wadi katika bunge la kaunti ya Nakuru amewataka wakaazi wa taarafa ya Elburgon na Molo kuchukua jukumu la kuendesha vita dhidi ya pombe haramu na dawa za kulevya wenyewe haswa msimu huu wa likizo.
Mwakilishi wa wadi ya Elburgon Florence Wambui Njoroge amejutia kwamba pombe haramu na dawa za kulevya haswa bhangi kuwa tishio kwa vijana wengi katika kaunti ya Nakuru na kwamba kunahaja ya wadau wote kuendeleza kampeini dhidi ya maovu hayo.
Mwakilishi huyo alikuwa akiongea katika eneo la Kasarani siku ya jumapili.
Kiongozi huyo amesema licha ya rais Uhuru Kenyatta kuwataka viongozi wote na maafisa wa serikali kukabiliana na pombe haramu na dawa za kulevya bado biashara hiyo inaendelea huku watu wengi wakiendelea kuadhirika.
Bi Njoroge alisema: “Wanaume na vijana wengine wanaoendeleza dhuluma kama unajisi, wengi hutumia dawa za kulevya kama marijuana na pombe haramu ambazo huwafanya wajihisi shupavu. Kwa hivyo, tukitaka kusafisha kijiji chetu na kaunti yetu, lazima tushirikiane kumaliza pombe na mihadarati pahali tulipo, kisha tuite polisi.”