Share news tips with us here at Hivisasa

Wakaazi wa eneo la Kiunga katika kaunti ndogo ya Lamu Mashariki kaunti ya Lamu sasa wanaunga mkono mpango wa serikali wa kuekeza miradi wa bandari ya pili nchini Kisiwani Lamu.

Wakaazi hao wakiongozwa na kiongozi wa vijana Kisiwani Lamu Mohammed Salim wamesema kuwa mpango huo huenda ukasaidia kuimarisha uchumi wa eneo hilo sambamba na kuwepo kwa nafasi za ajira kwa asilimia kubwa.

Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Ijumaa baada ya kukutana na viongozi wa vijana katika kaunti ya Mombasa, Salim amesema kuwa iwapo serikali pamoja na wasimamizi wa halmashauri ya Bandari nchini KPA wataafikiana vyema na kuwafidia wakaazi watakaothirika na mradi huo basi wengi wataunga mkono kwani utata uliyopo utasitishwa.

Amesema kuwa kujengwa kwa bandari ya Lamu na ile ya Kisiwa cha Shimoni kutawavutea wengi wa wawekezaji nchini na maswala ya kibiashara, uchumi, ajira na uwekezaji utaimarika zaidi.

“Tunaounga mkono hatua ya serikali na KPA lakini tunaomba maswala ya fidia yatekelezwe bila kutegemea upande wowote wala kuwadhuluma baadhi ya jamii Fulani," alisema Salim.

Kuali ya Kiongozi huyo wa vijana kaunti ya Lamu imejiri baada ya Kaimu Mkurugenzi mkuu wa halmshauri ya bandari nchini KPA Catherine Wairi kusema kuwa mikakati mwafaka imeidhinishwa na ujenzi wa Lapset na bandari katika kisiwa cha Shimoni utatekelezwa.