Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakaazi wa maeneo ya Shika Adabu kaunti ya Mombasa wamewataka wanasiasa kusitisha shughuli za kampeni za mapema za uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 na kuwatimizia ahadi walizozitoa wakati wa kuchaguliwa kwao miaka minne iliyopita.

Wakiongozwa na mzee wa mtaa eneo hilo Mzee Mohammed, wakaazi wamelalamikia ukosefu wa maji safi, usalama, ujenzi wa barabara miongoni mwa ahadi walizotoa na bado hawajatimiza hata robo yake.

"Tunawasihi wanasiasa hawa kukoma kampeni za mapema na kufanya kazi. Tumechoshwa na ahadi za uwongo na mwaka wa 2017 zitajulikana mbivu na mbichi," alisema Mzee.

Kwa sasa eneo hilo limesahaulika kimaendeleo na hata hospitali ya serikali iliyoko eneo hilo pia halina dawa za kutosha kwani wagonjwa huagizwa wanunue kwenye duka za dawa kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo.

Wameitaka serikali kuhakikisha kuwa wanasiasa wamechaguliwa kwa utendaji kazi wao ifikapo uchaguzi mkuu na kuwaondoa wazembe ili kunufaika na miradi na hata fedha ambazo hutolewa na serikali kuu pamoja na kaunti.