Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya kaunti ya Mombasa imekosoa hatua ya serikali kuu kupitia kwa maafisa wake wa Ardhi pamoja na kamati inayosimamia ugavi wa shamba la Waitiki eneo la Likoni kuwa wakazi katika shamba hilo watalipa shilingi elfu mia moja themanini na mbili kama ada ya shamba hilo.

Kaimu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Mpangilio wa Mji Kaunti ya Mombasa Antony Njaramba alisema utaratibu unaotumika wa kulipa ada hiyo kwa familia elfu kumi na moja ni ukiukaji wa haki kwani wakazi hao hawana fedha.

Kwenye kikao na wanabahari mjini Mombasa siku ya Jumatano, Bw Njaramba alisema serikali ya kaunti inaunga mkono hatua ya utoaji wa hati miliki za ardhi katika shamba hilo lakini ada hiyo inafaa kupunguzwa iwapo serikali imeamua wakazi hao kugharamikia mambo madogo madogo.

"Sisi tumekuwatukijua kuwa shamba litapimwa na masorovea kisha wakazi wetu wapewa hati miliki zao, swala la kulipa ada ya shilingi elfu 182 kwa kila familia ya zaidi ya watu elfu 11 hiyo hatukua tunafahamu lakini la msingi wakaazi wetu wapunguziwe ghaharama hiyo," alieza Njaramba.

Njaramba aliambia serikali kulifikiria swala hilo kwa kina ili kuona kwamba wananchi hao wanasaidika kwani wengi wao hawana uwezo wa kupata fedha hizo.

Kauli ya kiongozi huyo imejiri siku moja tu baada ya Afisa wa Serikali anayesimamia shughuli za usorovea katika shamba hilo Joseph Kinyiri kusema kuwa ada hiyo italipwa katika kipindi cha miaka mitatu kugharamikia shughuli za usorovea katika shamba hilo la zaidi ya ekari 930.